The United Republic of Tanzania
Ministry of Education Science and Technology
Vocational Education and Training Authority
Skilled Labour Force The Future of Tanzania
VETA - GOROWA KUWA KITUO CHA MAFUNZO YA UMAHIRI WA UFUNDI STADI NGAZI YA TATU KWA WASICHANA
Posted on: Wednesday, 18 June 2025
VETA - GOROWA KUWA KITUO CHA MAFUNZO YA UMAHIRI WA UFUNDI STADI NGAZI YA TATU KWA WASICHANA
Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA), Kanda ya Kati imezindua rasmi mpango wa kukifanya Chuo cha VETA Gorowa kilichopo mjini Babati, Manyara kuwa kituo maalum cha utoaji Mafunzo ya umahiri katika Mafunzo ya Ufundi Stadi ngazi ya III kwa wasichana nchini.
Akiongea na waandishi wa habari katika ukumbi mdogo wa mikutano wa chuo cha VETA-Gorowa wakati wa tukio la uzinduzi wa mpango huo, leo tarehe 18 Juni, 2025 Mkurugenzi wa VETA Kanda ya Kati, Ramadhani Mataka amesema, pamoja na kuongeza umahiri wa wahitimu wa ufundi stadi kwa ajili ya kuhudumia viwanda na sekta nyingine za uchumi, mpango huo pia ni sehemu ya mkakati wa VETA kujiandaa kuzalisha walimu wengi kwa ajili ya vyuo vya VETA vinavyoendelea kujengwa kote nchini na shule za sekondari za mkondo wa amali.
Kwa upande wake Mkuu wa chuo cha VETA-Gorowa, Joshua Benge Matagane amesema tukio la uzinduzi wa mpango limelenga kuujulisha umma wa Watanzania kuwa ifikapo mwezi Julai, 2025 chuo hicho kitaanza kutoa rasmi mafunzo ya muda ngazi ya tatu, huku walengwa wakiwa ni wasichana.
"Tunatarajiwa kuanza kutoa mafunzo hayo kwa wasichana 80 katika fani tatu, ambazo ni Umeme, Ufundi Bomba na Ushonaji, Ubunifu na Teknolojia ya Nguo kwa mwaka huu, 2025,” amesema.
Matagane ameongeza kuwa ifikapo mwakani, Januari, 2026 chuo hicho kitaongeza kozi nyingine nne za muda mrefu kwa ngazi ya tatu ikiwepo Uandaaji Chakula, TEHAMA, Utunzaji wa Bustani za Mbogamboga na Utunzaji wa Mifugo na Mazao yake, ambapo wasichana 120 wanatarajiwa kujiunga nazo.