The United Republic of Tanzania
Ministry of Education Science and Technology
Vocational Education and Training Authority
Skilled Labour Force The Future of Tanzania
Mkurugenzi Mkuu VETA aahidi ubunifu zaidi utoaji wa mafunzo ya ufundi stadi
Posted on: Saturday, 06 July 2024
Mkurugenzi Mkuu VETA aahidi ubunifu zaidi utoaji wa mafunzo ya ufundi stadi
Aihakikishia jamii utayari wa VETA kuwahudumia watanzania wa makundi yote
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi, CPA Anthony Kasore, amesema VETA itaendelea kubuni mbinu mbalimbali za utoaji mafunzo ili kuhakikisha watanzania wanapata mafunzo bora yanayoendana na mahitaji halisi ya soko la ajira.
CPA Kasore amesema hayo leo tarehe 6 Julai, 2024 alipozungumza na waandishi wa habari na kukutana na wananchi mbalimbali waliotembelea banda la VETA kwenye Maonesho ya 48 ya Biashara ya Kimataifa Dar es Salaam.
Ametaja uanzishwaji wa mtaala wa Mafunzo kwa Wafanyakazi wa Majumbani kama njia mojawapo ya kuitikia mahitaji ya soko la ajira la kuwa na watanzania wenye ujuzi wa kazi hiyo unaotambulika katika ngazi za Kimataifa.
“kazi yetu ni kuhakikisha tunatoa mafunzo katika sekta mbalimbali kulingana na mahitaji ya soko la ajira na tumejipanga vyema katika kuanzisha programu kadiri ya mahitaji hayo,”amesema
CPA Kasore amesema miongoni mwa mitaala mipya iliyoanzishwa hivi karibuni kuwa ni mtaala wa kozi ya Utengenezaji wa Vifaa Tiba itakayoanza kutolewa katika vyuo vya VETA vya mikoa ya Mara na Geita ambapo awali kozi hiyo ilikuwa ikitolewa katika vyuo vya ngazi ya elimu ya juu pekee.
Amewakaribisha wadau mbalimbali kushirikiana na VETA katika kuboresha utoaji mafunzo ya ufundi stadi na kuwafikia watanzania wengi zaidi huku akiahidi utayari wa VETA kutoa mafunzo hayo kwa umahiri na ubora.
CPA Kasore amehimiza wanancho kutembelea banda la VETA lililopo Mtaa wa Viwanda banda namba 14 kupata taarifa za kina juu ya fursa za mafunzo zinazopatikana kwenye vyuo vya VETA nchini na kujionea shughuli zinazofanywa na wanafunzi, walimu na wahitimu wa VETA.