The United Republic of Tanzania
Ministry of Education Science and Technology
Vocational Education and Training Authority
Skilled Labour Force The Future of Tanzania
MAAFISA RASILIMALI WATU VETA WANOLEWA NAMNA YA UENDESHAJI MASHAURI YA KINIDHAMU
Posted on: Thursday, 03 October 2024
Mameneja na Maafisa wa Rasilimali Watu na Utawala kutoka Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA), wamepatiwa mafunzo elekezi kuhusiana na namna ya uendeshaji wa mashauri ya kinidhamu.
Mafunzo hayo ya siku tatu yamefanyika kuanzia tarehe 25 hadi 27 Septemba, 2024 katika ukumbi wa mikutano wa Mt. Gaspar, jijini Dodoma.
Mkurugenzi Mkuu wa VETA, CPA Anthony Kasore amewaasa washiriki wa mafunzo hayo kuzingatia taratibu za kushughulikia masuala ya nidhamu akitegemea mashauri ya nidhamu yanafanyiwa kazi kwa ufanisi baada ya mafunzo hayo, badala ya kuishia kuyapeleka Makao Makuu.
“Mafunzo haya ni muhimu, naamini yatapunguza changamoto za muda mrefu za utatuzi wa masuala ya nidhamu. Aidha naomba mkasikilize kero za watumishi na kuzitatua kwa kutoa haki sawa,” CPA Kasore amesema
Amewaomba kwa kutoa ushauri ngazi za juu katika mashauri ambayo yatashindikana kutatuliwa katika maeneo yao.
Akizungumza katika mafunzo hayo, Kaimu Mkurugenzi wa Rasilimali Watu na Utawala wa VETA, Eniart Mahundi ametumia jukwaa hilo kuwakumbusha Mameneja Rasilimali Watu wa Kanda za VETA na Maafisa Rasilimali Watu kuacha kufanya kazi kwa mazoea badala yake wanapaswa kuwajibika ipasavyo katika maeneo yao ya kazi na kuwa na kuwaheshimu watumishi walio chini yao.
Kaimu Mkurugenzi, Kitengo cha Miongozo na Mafunzo, Ofisi ya Rais, Tume ya Utumishi wa Umma, Robert John Lwanji amesema, Afisa Rasilimali Watu anapaswa kuzingatia sheria, kanuni na miongozo ya Utumishi wa Umma juu ya namna ya kushughulikia masuala ya nidhamu.
Lwanji amebainisha makosa mawili ambayo mtumisha anaweza kushitakiwa ambayo ni makosa mazito kwayo yanaweza kupelekea kufukuzwa kazi, kushushwa cheo au kukatwa mshahara asilimia 15 katika kipindi cha miaka mitatu mfululizo na makosa mepesi ambayo mtumishi ataweza kupewa onyo, karipio au kuondolewa nyongeza ya mshahara (Increment).
Amesema kabla ya kumchukulia mtumishi hatua ya kinidhamu ni vyema mamlaka ya nidhamu kufanya uchunguzi wa awali ili kubaini ukweli kuhusiana na tuhuma alizonazo na wakati wa uchunguzi mtumishi anaweza kupumzishwa kutekeleza majukumu yake na atalipwa mshahara wake na ataweza kuja kazini au vinginevyo kwa kipindi cha siku tisini (90).
“Ni marufuku kumsimamisha kazi mtumishi hadi awe amepewa hati ya mashtaka na akisimamishwa kazi atapaswa kulipwa mshahara wote hadi shauri lake litakapohitimishwa na endapo mtumishi akiwa na kesi mahakamani anaweza kusimamishwa kazi,” Lwanji amefafanua.
Amesema mtumishi ana haki ya kukata rufaa kwenye Tume ya Utumishi wa Umma ndani ya siku 45 na kama hataridhika na maamuzi hayo pia anaweza kukata rufaa kwa Mhe. Rais na maamuzi ya Rais asiporidhishwa nayo ana haki ya kukata rufaa mahakamani.
Aidha, amewaasa watumishi kuzifahamu na kuzitumia sheria, kanuni na taratibu za kushughulikia masuala ya nidhamu pia kufahamu kuwa si kila mtu anaweza kumchukulia hatua za kinidhamu mtumishi wa umma.