The United Republic of Tanzania
Ministry of Education Science and Technology
Vocational Education and Training Authority
Skilled Labour Force The Future of Tanzania
WANAWAKE 664 DODOMA WANUFAIKA NA MAFUNZO KUPITIA USHIRIKIANO WA VETA NA WANAWAKE NA SAMIA
Posted on: Wednesday, 20 August 2025
WANAWAKE 664 DODOMA WANUFAIKA NA MAFUNZO KUPITIA USHIRIKIANO WA VETA NA WANAWAKE NA SAMIA
Jumla ya wanawake 664 wamenufaika na mafunzo ya ufundi stadi kwenye chuo cha VETA Dodoma katika kipindi cha Machi hadi Agosti 2025, kupitia mpango wa ushirikiano kati ya VETA na taasisi ya Wanawake na Samia.
Mafunzo hayo ya muda wa mwezi mmoja, yamehusisha kozi za Ususi na Urembo; Upambaji wa Matukio na Sherehe Mbalimbali; Huduma ya Mapokezi; Upishi; Huduma za Chakula na Vinywaji; Usafi Wa Majumbani na Hotelini na Ushonaji, Ubunifu na Teknolojia ya Nguo.
Akizungumza wakati wa mahafali ya wahitimu wa kozi hizo, jana tarehe 18 Agosti, Waziri wa Madini, Mheshimiwa Anthony Mavunde ameipongeza VETA kwa kufanikisha kutoa mafunzo kwa kundi hilo la wanawake na kusema mafunzo hayo yatawawezesha kutumia vyema fursa za kiuchumi zilizopo sasa katika mkoa wa Dodoma.
Amesema jiji la Dodoma sasa linakuwa kwa kasi kutokana na kuwa makao makuu ya nchi na watu wengi kuhamia, hivyo kufungua milango mipya ya fursa za kiuchumi ambazo wananchi wa Dodoma lazima wazitumie ipasavyo.
Amesema fursa hizo zinahitaji ujuzi. Lakini kwa kujifunza kupitia VETA na taasisi kama hii ya Wanawake na Samia, tutahakikisha kwamba wanawake na vijana wa Dodoma wanakuwa mstari wa mbele kunufaika na fursa hizi.
“Bila ujuzi, tutashuhudia wageni kutoka mikoa mingine wakitumia nafasi ambazo zingetumiwa na wananchi wa Dodoma. Ni muhimu tukajiandaa kutumia fursa hizi, badala ya kuwa wapenzi watazamaji,” amesema.
Mavunde ameahidi kuwapatia wanawake hao mtaji wa shilingi Milioni 10, nakushirikiana na Ofisi ya Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma na Mkuu wa wilaya ya Dodoma kuboresha eneo kwa ajili ya kufanyia shughuli zao za biashara.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Bi Rosemary Senyamule amesema kuwa mafunzo hayo hayajanufaisha kundi la wanawake na Samia pekee bali kila mwanamke aliyejitokeza kutaka ujuzi.
“Taasisi ya Wanawake na Samia ilikuwa na kazi kubwa ya kuratibu wanawake wanaojitokeza kupata mafunzo, hivyo mafunzo haya yametolewa kwa kila mwanake aliyehitaji ujuzi” amesema Senyamule.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa VETA CPA Anthony Kasore amesema shabaha ya awali katika mpango huo ilikuwa nikuwafikia wanawake 3000, lakini kutokana na mwitikio mkubwa, VETA sasa imelenga kuwafikia wanawake 15000 nchini.
“Sisi VETA tutahakikisha tunatoa mafunzo kwa kadiri wananchi wanavyohitaji tunafungua milango kwa wananchi kuja kutuambia tunataka mafunzo haya sisi tupo tayari kuwapatia mafunzo” amesema Kasore.
Aidha Mkuu wa chuo cha VETA Dodoma Deodatus Orotha akisoma taarifa fupi za utoaji mafunzo hayo amesema mafunzo hayo yalianza kutolewa tarehe 26 Machi, 2025 kwa kundi hilo ambapo hadi jana wanawake 664 wamehitimu nakusema kuwa kwa mkoa wa Dodoma sasa wamelenga kuwafikia wanawake 2000.