The United Republic of Tanzania
Ministry of Education Science and Technology
Vocational Education and Training Authority
Skilled Labour Force The Future of Tanzania
VETA Yasaini Makubaliano na RES Inspection & Engineering Services Ltd Kutoa Mafunzo
Posted on: Wednesday, 20 August 2025
VETA Yasaini Makubaliano na RES Inspection & Engineering Services Ltd Kutoa Mafunzo maalum yanayotambulika Kimataifa ya Uundaji na Uungaji Vyuma na Ukaguzi
Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) imeingia makubaliano rasmi na kampuni ya RES Inspection & Engineering Services Ltd kwa lengo la kuanzisha mafunzo maalum yatakayokidhi ithibati za kimataifa ((International Certification) katika fani ya Uundaji na Uungaji wa Vyuma na Ukaguzi ).
Makubaliano hayo yanalenga kuongeza ajira na kupunguza utegemezi wa wataalamu kutoka nje ya nchi katika miradi mikubwa ya miundombinu.
Akizungumza wakati wa hafla ya utiaji saini, Mkurugenzi Mkuu wa VETA, CPA Anthony Kasore, amesema kuwa mafunzo hayo yataanza kutolewa katika vyuo vya VETA Dodoma, Moshi na Geita.
“Tunaenda kuanza kutoa mafunzo haya kwa kushirikiana na wataalamu wa kampuni ya RES ambao wana uzoefu mkubwa katika sekta ya Uungaji na Ukaguzi wa Vyuma. Kupitia ushirikiano huu, walimu wetu watajengewa uwezo kufundisha kwa viwango vya kimataifa,” amesema Kasore.
Aidha, amebainisha kuwa hadi sasa hakuna kituo chochote cha mafunzo katika ukanda wa Afrika Mashariki kinachotoa mafunzo haya yenye ithibati ya kimataifa, hivyo ushirikiano huu unaleta fursa kubwa kwa Tanzania kuwa kitovu cha mafunzo ya aina hii katika kanda.
“Hili ni jambo muhimu kwa maendeleo ya vijana wetu, hasa ikizingatiwa miradi mikubwa ya kimkakati kama ujenzi wa bomba la mafuta na gesi. Hatutaki kuendelea kutegemea wataalamu kutoka nje ya nchi,” ameongeza Kasore.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi wa VETA, Dkt. Abdallah Ngodu, amesema kuwa makubaliano hayo yatajikita katika maeneo kadhaa muhimu ikiwemo uandaaji wa mitaala, uthibitishaji wa ubora wa mafunzo, ujenzi wa uwezo kwa walimu, ushauri wa kitaalamu na uhusiano na viwanda ili kuhakikisha wahitimu wanapata ajira.
Mkurugenzi wa RES Inspection & Engineering Services Ltd, Ndugu Sospeter Lugembe, ameeleza kuwa kwa sasa kuna vyuo vinne tu barani Afrika vinavyotoa mafunzo haya kwa viwango vya kimataifa — Afrika Kusini, Misri, Morocco na Tunisia — na kwamba Tanzania inaweza kuwa ya tano kupitia ushirikiano huu.
“Mafunzo haya yatapunguza gharama kwa Watanzania waliokuwa wanalazimika kwenda nje ya nchi kupata ujuzi huu, na pia yatafungua mlango kwa wanafunzi kutoka nchi jirani kuja kusomea hapa,” alisema Lugembe.
Kwa upande wake, Erick Masele kutoka RES ameongeza kuwa uhitaji wa wataalamu waliobobea kwenye maeneo haya ni mkubwa hasa kwa miradi mikubwa, viwanda, matenki ya kuhifadhia mafuta, maji, na kemikali, ambayo baadhi yanahitaji uungaji wa vyuma kwa ustadi wa hali ya juu.
Kampuni ya RES Inspection & Engineering Services Ltd inajihusisha na huduma za ukaguzi wa vyuma kwa kutumia teknolojia ya NDT, pamoja na kutoa mafunzo maalum kwa wachomeleaji (welders) na kuwapatia vyeti vinavyotambulika kimataifa.
Makubaliano haya yanaashiria hatua kubwa kwa VETA katika kukuza ujuzi wa vijana na kuwapa nafasi ya kushiriki kikamilifu katika miradi ya kimkakati kitaifa na kimataifa.