The United Republic of Tanzania
Ministry of Education Science and Technology
Vocational Education and Training Authority
Skilled Labour Force The Future of Tanzania
CPA KASORE ASISITIZA UTENDAJI KAZI KIMKAKATI KUCHOCHEA MAGEUZI ELIMU YA UFUNDI STADI
Posted on: Monday, 22 September 2025
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA), CPA Anthony Kasore, amewataka Wakuu wa Vyuo vya VETA kote nchini kufanya kazi kimkakati ili kuleta matokeo chanya katika ukuzaji wa elimu na mafunzo ya ufundi stadi nchini.
Akifunga kikao cha pili cha wakuu wa vyuo hivyo kilichofanyika kwenye hoteli ya VETA, Njiro jijini Arusha, jana tarehe 20 Septemba, 2025, CPA Kasore amesema VETA ni taasisi ya kimkakati inayopaswa kuchochea maendeleo ya kijamii na kiuchumi nchini.
Amesema ni muhimu kuandaa mipango ya muda mrefu na mfupi inayoendana na Dira ya Taifa ya Maendeleo na mikakati mingine ya Kitaifa, kushirikiana na wadau kuboresha miundombinu na huduma, pamoja na kutumia ujuzi kusaidia jamii zinazozunguka vyuo.
"Rais wetu amekuwa mstari wa mbele kusisitiza umuhimu wa kutoa ujuzi kwa Watanzania ili waweze kujiajiri, kuajiriwa na hata kuajiri wengine. Wakati wa uzinduzi wa Chuo cha Ufundi Stadi cha Mkoa wa Kagera," amesema.
Aidha, amewataka kushirikiana na wadau wa maendeleo na kutumia diplomasia ya kiuchumi ili kupata rasilimali muhimu za kuboresha miundombinu na huduma za mafunzo.
“Tuondoe fikra kwamba kila kitu lazima kiletwe na serikali. Shaurianeni, andikeni mapendekezo na tafuteni wadau wa kusaidia vyuo vyenu. Tukitumia rasilimali zilizopo vizuri, tutaongeza tija na kuimarisha mafunzo ya ufundi,” amesema.
Vilevile, CPA Kasore aliwasihi viongozi hao kuandaa viongozi wengine ndani ya taasisi zao ili kuendeleza mafanikio ya vyuo hata wanapostaafu au kubadilishwa na kusisitiza kuwa kiongozi bora lazima awe tayari kusikiliza na kushirikisha wengine katika maamuzi ya kimkakati.
Kwa upande wake, Mkuu wa Chuo cha VETA Hoteli na Utalii, Bw. Magu Mabele, alisema kikao hicho kimekuwa na mchango mkubwa katika kujenga uelewa wa pamoja na kuimarisha utendaji wa vyuo, hatua inayosaidia kufanikisha mageuzi ndani ya taasisi hiyo.